Genesis 37

Ndoto Za Yosefu

1 aYakobo akaishi Kanaani katika nchi ambayo baba yake alikuwa ameishi.

2 bZifuatazo ni habari za Yakobo.

Yosefu, kijana wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga makundi ya kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake wa mama wengine, yaani wana wa Bilha na wana wa Zilpa wake za baba yake, naye akawa akimletea baba yake taarifa mbaya kuhusu hao ndugu zake.

3 cBasi, Israeli akampenda Yosefu kuliko yeyote miongoni mwa kaka zake, kwani ni mwanawe wa uzeeni, akamshonea joho lililorembwa vizuri sana. 4 dNdugu zake walipoona kwamba baba yao anampenda Yosefu kuliko yeyote mwingine miongoni mwao, walimchukia na hawakusema naye neno lolote jema.

5Yosefu akaota ndoto, naye alipowaeleza ndugu zake, wakamchukia zaidi. 6Akawaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota: 7 eTulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani, ghafula mganda wangu ukasimama wima, wakati miganda yenu ikiuzunguka na kuuinamia.”

8 fNdugu zake wakamwambia, “Wewe unakusudia kututawala? Hivi kweli wewe utatutawala sisi?” Wakaongeza kumchukia zaidi kwa sababu ya ndoto yake pamoja na yale aliyowaambia.

9Kisha akaota ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine, wakati huu jua, mwezi na nyota kumi na moja zilikuwa zinanisujudia.”

10 gAlipomwambia baba yake pamoja na ndugu zake, baba yake akamkemea akisema, “Ni ndoto gani hii uliyoota? Hivi kweli mama yako na mimi na ndugu zako tutakuja kukusujudia wewe hadi nchi?” 11 hNdugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akaliweka jambo hilo moyoni.

Yosefu Auzwa Na Ndugu Zake

12 iBasi, ndugu zake walikuwa wamekwenda kuchunga makundi ya baba yao karibu na Shekemu, 13 jnaye Israeli akamwambia Yosefu, “Kama ujuavyo, ndugu zako wanachunga makundi huko karibu na Shekemu. Njoo, nitakutuma kwao.”

Yosefu akajibu, “Vema sana, niko tayari.”

14 kKwa hiyo akamwambia, “Nenda uone kama mambo yote ni salama kwa ndugu zako na makundi, kisha uniletee habari.” Ndipo akamtuma Yosefu kutoka Bonde la Hebroni.

Yosefu alipofika Shekemu,
15mtu mmoja akamkuta akizungukazunguka mashambani na akamuuliza, “Unatafuta nini?”

16Akajibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Unaweza kuniambia wanachunga wapi makundi yao?”

17 lYule mtu akajibu, “Wamehama hapa. Nilisikia wakisema, ‘Twende Dothani.’ ”

Kwa hiyo Yosefu akawafuatilia ndugu zake na kuwakuta karibu na Dothani.
18 mNdugu zake walipomwona akiwa mbali, kabla hajawafikia, wakapanga shauri baya la kumuua.

19 nWakaambiana, “Yule mwota ndoto anakuja! 20 oNjooni sasa, tumuue na kumtupa katika shimo mojawapo na tuseme kwamba mnyama mkali amemrarua. Kisha tutaona matokeo ya ndoto zake.”

21 pReubeni aliposikia jambo hili, akajaribu kumwokoa kutoka mikononi mwao akasema, “Tusiutoe uhai wake. 22 qTusimwage damu yoyote. Mtupeni katika shimo lililoko hapa jangwani, lakini msimguse.” Reubeni alisema hivyo ili amwokoe kutoka mikononi mwao, kisha amrudishe nyumbani kwa baba yake.

23 rKwa hiyo Yosefu alipowafikia ndugu zake, walimvua lile joho lake, lile joho lililorembwa vizuri alilokuwa amevaa. 24 sKisha wakamchukua wakamtupa katika shimo. Wakati huo shimo lilikuwa tupu, halikuwa na maji ndani yake.

25 tWalipokaa ili wale chakula chao, wakainua macho wakaona msafara wa Waishmaeli ukija kutoka Gileadi. Ngamia wao walikuwa wamepakizwa mizigo ya vikolezo, uvumba na manemane, nao walikuwa njiani kuvipeleka Misri.

26 uYuda akawaambia ndugu zake, “Tutafaidi nini ikiwa tutamuua ndugu yetu na kuificha damu yake? 27 vNjooni, tumuuze kwa hawa Waishmaeli. Tusimguse, kwa kuwa hata hivyo yeye ni ndugu yetu, nyama yetu na damu yetu wenyewe.” Ndugu zake wakakubali.

28 wKwa hiyo wale wafanyabiashara Wamidiani walipofika pale, ndugu zake wakamtoa Yosefu kutoka kwenye lile shimo, na kumuuza kwa shekeli ishirini
Shekeli 20 ni sawa na gramu 200.
za fedha kwa wale Waishmaeli, ambao walimpeleka Misri.

29 yReubeni aliporudi kutazama kwenye lile shimo na kuona kwamba Yosefu hayupo, alirarua nguo zake. 30 zAkawarudia ndugu zake na kusema, “Kijana hayuko mle! Nielekee wapi sasa?”

31Kisha wakalichukua lile joho la Yosefu, wakachinja mbuzi na kulichovya katika damu. 32Wakalichukua lile joho lililorembwa vizuri na kulipeleka kwa baba yao na kusema, “Tumeliokota hili joho. Uchunguze uone kama ni la mwanao.”

33 aaBaba yao akalitambua akasema, “Hili ni joho la mwanangu! Mnyama mkali amemrarua. Hakika Yosefu ameraruliwa vipande vipande.”

34 abKisha Yakobo akararua nguo zake, akavaa nguo ya gunia na kumwombolezea mwanawe kwa siku nyingi. 35 acWanawe wote na binti zake wakaja kumfariji, lakini hakukubali kufarijiwa. Akasema, “Hapana, nitamwombolezea mwanangu mpaka nimfikie kaburini.” Kwa hiyo baba yake akaendelea kumlilia.

36 adWakati ule ule, Wamidiani wakamuuza Yosefu huko Misri kwa Potifa, mmojawapo wa maafisa wa Farao, aliyekuwa mkuu wa ulinzi.

Copyright information for SwhNEN